Kwa kuondokewa na Sheikh Ali Jumaa Mayunga, jamii ya Kiislamu Afrika Mashariki imepoteza hazina kubwa ya elimu na hekima. Hata hivyo, elimu yake, maandiko yake na athari zake zitaendelea kuishi na kuwanufaisha vizazi vijavyo, kama sadaka jariya isiyokatika matunda yake. Mwenyezi Mungu amsamehe madhambi yake, ampanulie kaburi lake, na amjaalie daraja za juu katika Pepo pamoja na waja Wake wema.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Waumini wa Kiislamu, Masheikh, na wadau wa elimu ya Dini kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania na Afrika Mashariki wameungana siku ya Ijumaa kumuaga rasmi Marehemu Sheikh Ali Jumaa Mayunga, Mwanachuoni Mashuhuri na nguzo muhimu ya maarifa ya Kiislamu katika eneo hili. Mazishi na Maziko yake yamefanyika baada ya Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa katika Masjid Amirul Muuminin Ali bin Abi Talib (a.s), iliyopo Magomeni, jijini Dar es Salaam, katika mazingira ya huzuni, heshima na dua mbalimbali za kumrehemu.
Sheikh Ali Jumaa Mayunga amebaki kuwa alama muhimu katika historia ya elimu ya Kiislamu Afrika Mashariki, kutokana na mchango wake mkubwa katika nyanja ya utafiti, ufundishaji na uandishi. Alijulikana sana kwa juhudi zake za kueneza maarifa sahihi ya Dini Tukufu ya Kiislamu, hususan kupitia kazi zake za kielimu zilizoandikwa kwa lugha fasaha, hoja thabiti na dalili makini. Miongoni mwa athari zake zitakazodumu kwa muda mrefu ni tafsiri yake maarufu ya Qur’ani Tukufu kwa lugha ya Kiswahili, kazi ambayo imekuwa rejea muhimu kwa wanafunzi, walimu na wapenzi wa Qur’ani katika ukanda huu.
Mazishi hayo yamehudhuriwa na umati mkubwa wa waombolezaji wakiwemo masheikh, walimu, maustadhi, wanafunzi, ndugu, jamaa na marafiki kutoka Dar es Salaam na mikoa mingine ikiwemo Arusha, Tanga, Bagamoyo, Lindi na Kibaha. Uwingi wa waliojitokeza unaakisi nafasi na heshima kubwa aliyokuwa nayo marehemu katika jamii ya Kiislamu na kielimu.

Miongoni mwa viongozi wa dini na taasisi waliohudhuria ni Dr. Ali Taqavi, Rais wa Jamiat Al-Mustafa (s) – Dar es Salaam, Tanzania, pamoja na viongozi na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za Kiislamu. Wote kwa pamoja walishiriki katika kuusindikiza mwili wa marehemu, kumuombea dua ya maghfira na rehema, na kumuombea afufuliwe pamoja na Mtume Muhammad (s.a.w.w) na Ahlul-Bayt wake watukufu.

Kwa kuondokewa na Sheikh Ali Jumaa Mayunga, jamii ya Kiislamu Afrika Mashariki imepoteza hazina kubwa ya elimu na hekima. Hata hivyo, elimu yake, maandiko yake na athari zake zitaendelea kuishi na kuwanufaisha vizazi vijavyo, kama sadaka jariya isiyokatika. Mwenyezi Mungu amsamehe madhambi yake, ampanulie kaburi lake, na amjaalie daraja za juu katika Pepo pamoja na waja Wake wema.
Your Comment